Makatazo ya Rushwa kwa mujibu wa Biblia, Quran tukufu na Hadithi za Mtume Muhammad (s.a.w)

zanzibatimes-staff
By -
0


Kuhusu Mwandishi:

Mwandishi wa kitabu hiki anaitwa mzee  Yusuph Rajab Makamba ni Katibu mkuu mstaafu wa chama cha mapinduzi, mkuu wa mkoa mstaafu wa mkoa wa Dar es salaam. Na pia kwa sasa ni baba wa Waziri wa mambo ya nje na uhusiano wa Afrika Mashariki, January Makamba.


Mwandishi amekiandika kitabu hiki mwaka 2003, akiwa ni mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, mjumbe wa halmashauri kuu ya Taifa ya Chama Cha Mapinduzi na mwenyekiti wa Baraza la Taifa la Usalama Barabarani.


Kwanini hiki Kitabu?

Mosi; hiki kimepata kuandikwa dibaji na Mheshimiwa Rais mstaafu Mkapa kipindi hiko akiwa ndio Rais wa jamhuri ya muungano wa Tanzania. Na kiongozi mkuu dhidi ya upambanaji wa rushwa nchini.


Pili; “ Makamba ameilenga, ameizingatia na ameishirikisha ya sasa na ijayo kwa ‘staili’ nyepesi na ya aina yake. Ni rejea muhimu kwa shule zote na vyuo vyote.” profesa  

Mwijarubi Muhongo — idara ya jiolojia, chuo kikuu cha Dar es Salaam


Tatu;hiki ni kitabu kinacho onyesha kwa ufasaha na upevu wa hali ya juu jinsi rushwainavyokemewa si tu katika maandishi matakatifu, bali pia na viongozi wa dini na serikali. Maudhui ya kazi hii ni muhimu kwa jamii yote ya Tanzania.


Dondoo za utangulizi pamoja na dibaji



Rushwa ni adui wa haki


Rushwa ni adui wa haki, sitapokea wala kutoa rushwa – kiapo cha ahadi cha wana-CCM.


Nazi mbovu harabu ya nzima.


Rushwa ni haramu, ni dhami na ni chukizo mbele ya Mungu.


Tabia ya njoo kesho kwa jambo ambalo lingekwisha leo – huu ni urasimu usio na maana ambao unaashiria rushwa.


Imani ya dini ni silaha nzito kuliko silaha nyengine katika kupambana na rushwa.


Tuache kulalamika na kulaumiana na badala yake kila mmoja  wetu atimize wajibu wake, tukijua kwamba tuna dhamana mbele ya Mungu.


Deni la fadhila hulipwa kwa fadhila.


Vita dhidi ya rushwa haiwezi kufanikiwa kwa kutegemea serikali na sheria peke yake. Inahitaji mabadiliko ya tabia na mwamko mpya wa maadili yatokanayo na ucha – Mungu.


Usimsubiri mwenzako, kila mmoja wetu anao uwezo wa kuwa mfano wa kuigwa. Kila mmoja wetu adhamirie kuwa mpenda haki na asiyependa wala kuionea aibu rushwa ya aina yoyote ile. Tukifanya hivyo, tutaziimarisha imani zetu na kujenga jamii inayo heshimika, na inayo heshimu mafunzo na maagizo ya vitabu vyetu vItakatifu – na yenye kuyatenda mapenzi ya mwenyezi Mungu.


Rushwa hakika ni sumu, kaonya Mola muumba. ---  kwamba kila mla rushwa peponi hataingia. Na yamesema maandiko, rushwa inaua haki.


Makatazo ya Rushwa kwa mujibu wa Biblia.

Mungu alisema kuwa watumishi waliopewa dhamana ya kutoa huduma kwa wananchi wakiendekeza tabia ya kupokea rushwa, watapumbazika katika kutoa haki kwa wanao stahili, na kufanya upendeleo kwa wasio stahili.


Mungu aliwaelekeza wanasheria na mawakili wa enzi hizo wasipokee rushwa kwa sababu watashawishika kupindisha vifungu vya sheria ili kumpa haki yule asiye stahili na kufanya upendo kwa wasiostahili.


Mungu wa bibilia ni mwenye haki sana na wala hana upendeleo kwa mtu yeyote kwa hali hii, haiwezekani kwake yeye kupokea rushwa. Hata kama watumishi wake watadiriki kupokea rushwa kwa jina lake. Wanafanya hivyo pasipo yeye kushiriki.


Amelaaniwa mtu anaye pokea rushwa.


Rushwa haiwezi kumuokoa mwanamme aziniye na mke wa mtu.



Makatazo ya Rushwa kwa mujibu wa Q’uran na Hadithi za Mtume Muhammad(s.a.w) 


Uislamu ni dini, na dini yeyote ili iwe ya kweli lazima impe mafunzo na imlee mwanadamu kimwili na kiroho.


Dini ina mlea mwanadamu kiroho kwa kumfundisha mambo yote yatakayo mkurubisha kwa Mungu aliye muumba na imuelekeze namna ya kuyatekeleza maagizo ya Mwenyezi Mungu. Hali kadhalika dini inamlea mwanadamu kimwili, ina mmfundisha mambo yote yanayoweza kuleta madhara katika mwili wake, akili, na maisha yake kwa ujumla.


Katika mambo yanayofanya mwanadamu awe karibu na Mola wake, akubaliwe na jamii yake na wenzake – ni kuusimamisha uadilifu.


Kunyamazia maovu yatendwayo na baadhi yetu – si kheri kwetu hata kidogo. Bali ni kujihalalishia laana ya mwenyezi Mungu jambo ambalo ni hatari kwa jamii.


Mwenyezi Mungu amejiharamishia yeye mwenyewe kufanya dhulma na ameiharamisha kwa waja wake. Kwa kusema “ msidhulumiane”.


Kufanya dhulma kwa namna yeyote ile ni kuiasi amri ya mwenyezi Mungu.


Rushwa kwa kuwa ni dhulma ni moja ya mambo ambayo yanamzuilia mja kukubaliwa ibada zake na maombi yake kwa ujumla.


Rushwa imeharamishwa hata kama ni kwakuifikisha haki kwa mwenyewe kwani huku ni kupokea mali pasi na jambo lilio fanyika na inakuwa mbaya zaidi ikiwa ni kwa madhumuni ya kumdhulumu mtu na kumzuilia mwenye haki kupata haki yake.


Amesema mjumbe wa mwenyezi Mungu ”Yule ambaye tumemtuma kazi yoyote ile, tukampa malipo yake atakachokichukua baada ya hapo ni khiana” – Tunatahadharishwa kuto pokea zawadi  tunapo kuwa katika utumishi wa umma. Zawadi ni mali ya mwajiri. Malipo yetu ni mshahara yetu ya kila mwezi.


Wala rushwa hawana haya, na mtu anapokosa haya anakuwa amekosa sifa muhimu sana katika maisha kwani sifa hii kwa yule ambaye anakuwa nayo – anakuwa katika katika kinga kubwa sana,  na kutenda maovu na anapoikosa ndipo anakuwa hana mbele yake kizuizi chochote cha kufanya matendo maovu.


“Hakika katika yale ambayo wameyadiriki watu katika maneni na mafundisho ya mitume wa mwanzo ambayo yamejaa busara na mafunzo mengi katika maadili mema kama mafunzo hayo hayakukusaidia kukufanya mwenye difa ya haya – Basi kama hukuona haya fanya ulitkalo ( amepokea” — imepokelewa na Bukhary.

 

Ukweli ni kwamba kupokea na kutoa rushwa ni kielelezo kikubwa cha kuondokewa haya.


“Mwenyezi Mungu akimchukia mja huvua kwake haya na akivua kwake haya utamkuta mwenye kuchukiwa na  Mwenye kuchukiza na kuvuliwa kwake uaminifu huvuliwa kwake huruma na ikivuliwa kwake uaminifu huvuliwa kwake huruma huvuliwa kwake kwamba uisilamu na ikivuliwa kwake kwamba uislamu hutamkuta isipokuwa ni sheteani mwenye kuasi”  — imepokelewa na ibni Maja.  


Sura 2 aya 189; “ Enyi mlio amini, msiliane mali zenu kwa batili. Isipokuwa iwe biashara kwa kuridhiana baina yenu”.


Mtoa rushwa lengo lake kabisa ni kutaka haki isitendeke na dhulma ifanywe na anayepokea rushwa pia – Mungu hataki dhulma.


Rushwa ni kitu chochote kile au hali yeyote ile ya kuweza kumshawishi mtu ili afanye au asifanye jambo ambalo alitakiwe afanye au asifanye kwa mujibu wa sheria, taratibu, kanuni na miongozo iliyopo, na hivyo kujipatia kipato cha ziada au upendeleo wa kupata huduma asiyostahili.


Mojawapo ya madhara makubwa ya rushwa ni kudumaa kwa uchumi wetu, kuongezeka kwa umaskini na bila maskini kama matokeo yake.


Ili taifa liweze kupambana na kudhibiti rushwa ni muhimu sana uongozi wa juu ukawa mstari wa mbele, tusioneane haya katika mapambano haya kwa sababu kuoneana haya ni sawa na kuangamiza Taifa hili.


Tutii sheria na tumuogope Mungu kama tulivyokatazwa katika maandiko matakatifu – kutoa na kutopokea rushwa.


Nukuu za Viongozi wa dini kuhusu Rushwa.

“ Kutoa na kupokea rushwa ni kupiga vita haki na ni kula mali za watu kwa dhulma. Mwenye kufanya hayo anakula makaa ya moto jahanam hapa hapa duniani kabla ya akhera. Mwenyezi Mungu amemlaani mtoaji na mpokeaji” – Sheikh Issa Shabani Simba.


“Rushwa inaua kama ukimwi, kama vile UKIMWI ulivyo ‘Upungufu wa Kinga Mwilini’ vivyo hivyo na rushwa ni upungufu wa kinga rohoni” – Askofu Sylvester Gamanywa.


“Rushwa ingekuwa ni mtu, angekuwa na sura mbaya, mwenye harufu mbaya, angekimbiwa na watu” – sheikh Suleiman A. Kilemile


“Rushwa huwakosesha watu haki, husababisha fikra katika jamii. Fikra ni mbaya  kama alivyosema mwenyezi Mungu katika Quran sura ya pili aya 217 kwamba; “fitina ni mbaya kuliko kuua” – kwa hiyo wala rushwa  mwisho wao ni Jehanamu” — Sheikh Hamid Masoud Jengo.


“Katika Biblia rushwa imekatazwa mara kumi na nane kwahiyo, kwa mkristo kupokea na utoa rushwa ni kumgomea Mungu mara kumi na nane, ni kumkatalia Mungu, ni kumuasi Mungu mara kumi na nane. – ni dhambi ya uasi. (1 Yoh: 3 -4) – Neno la mungu katika Kutoka 23:8 linasema kuomba rushwa kkunapofua macho. Kwahiyo wanaotoa na kupokea rushwa wote ni vipofu. Ni vipofu wasiona haki; lakini pia ni vipofu katika mambo ya kiroho, mambo ya uhusiano wao na Mungu.” – Askofu Elineza E. Sendoro.


“Mungu yuko kinyume sana na rushwa kwa sababu; rushwa inawafanya hata wajane na yatima kuonewa, kudulumiwa na kunyimwa haki zao. Neno la Mungu husema, mtu mkuu au mtu yeyote anaye wadhulumu wajane na yatima – mungu hawezi kusikia maombi yake tena, ataficha kabisa uso wake asiuone. ( isaya 1: 15-17,23). Tukipiga vita rushwa, wajane na yatima watapata haki zao. Na hivyo kila raia atabarikiwa, na taifa zima litbarikiwa na Mungu.” – Askofu mkuu Zakaria Kakobe.



“Mkono unaotoa rushwa na ule unaopokea rushwa ni mkono wa shetani aliyelaaniwa. Jehanamu  ndio makazi yake. Tujiepushe na rushwa ili pepo ndiyo iwe makazi yetu.” — Sheikh Alhad Mussa Salum.


“Kutoa na kupokea rushwa ni sawa na kwafuta sheria watoa rushwa na wapokea rushwa ni sawa na wanyama  ambao huuishi bila sheria.” — Sheikh Mohammed iddi Mohammed.


“Kutoa na kupokea rushwa ni tendo la kuua, anayetoa rushwa anaunga mkono tendo la kuua na anayepokea rushwa ni muuaji. Na Mungu anasema usiue.”  — Askofu Volentino Mokiwa.


“Kupokea rushwa ni kusaliti sura ya mfano wa Mungu. Tunapokea kitu kidogo na kupoteza thamani kubwa.” — Kadinali Polycarp Pengo.


Nukuu za Viongozi wakuu wa Serikali.

“Juu ya mambo ya rushwa hatukuwa na utani na mtu hata kidogo. Rushwa ni jambo hatari sana, huwezi kununua haki; haki hainunuliwi, thamani yake ni shilingi ngapi hasa.”  – Mwl.J.K. Nyerere.


“Dhambi ya rushwa ni dhambi kongwe kuliko dhambi ya ukahaba… Mimi nafikiri dhambi ya rushwa ni kongwe karibu sawa na dhambi ya ukahaba… Naona kama ilivyo vigumu kufuta ukahaba katika jamii, ndivyo ilivyo vigumu kutafuta rushwa  lakini ubaya wa rushwa hupotosha haki ya wanyonge na kuleta hasara kwa taifa, upo wazi  na lazima rushwa ipigwe vita kwa bidii zetu zote… Rushwa  ni mbaya popote ilipo. Lakini rushwa ikijipenyeza  kwenye mahakama, ubaya wake unakuwa maradufu… Bwana mmoja anayopenda kuwatania wanasheria aliwatania wapo mawakili wa aina mbili; wale wanaojua sheria, na wale wanao mjua jaji.”.– B.W. Mkapa.


“Rushwa ni adui wa haki — mapato ya nchi yanapotea sehemu nyingi kutokana na rushwa. Tusikubali kulipa huduma amabazo zinapaswa kuwa bure. Rushwa inazidisha umaskini.. .Mzoea kazi ya udalali hawezi kazi ya duka….Wanaotoa  na kuopokea rushwa si watu wema na kwa hakika ni watu waovu na waliopotoka.” — Dr. Ali Shein



“Ufanisi wa shughuli za serikali utategemea sana kuwepo kwa misingi ya utawala bora… Rushwa huleta dhuluma na kero kwa wananchi na hasa wanyonge.  —  Amani Karume.


Hitimisho:

Nashukuru kwa muda wako katika kusoma uchambuzi wa kitabu hiki. Mwisho wa uchambuzi huu ni mwanzo wa uchambuzi wa vitabu vyengine. 


Kama uchambuzi huu umekuwa wenye mchango kwako, basi usisite kusambaza kwa rafiki zako.


Ahsante!



  



   


Tags:

Post a Comment

0Comments

Post a Comment (0)